Utangulizi: katika hii dunia kuna vitu ambavyo
havitakiwi kufa maana vinahitajika kizazi hadi kizazi hivyo unapopata jambo zuri, jitahidi
kuwafikishia wengine linaweza lisikusaidie wewe likamsaidia mwenzako, hapa
unaweza kujihamasisha wewe mwenyewe kwa
kusoma ujumbe huu na kuanza kuchukuwa hatua maana halisi ya kuweka masomo haya
ni wewe utumie na wengine kama mimi nilivyokuwekea wewe,
Je, huwa unajisemesha nini ukiwa mwenyewe? Je, huwa
unawaza nini ukipata sehemu ya utulivu ukawa mwenyewe? Je, huwa kila mara
unawaza nini? Je, huwa unapima kile unachowaza kama ni sehemu sahihi kwako
kabla ya kuendelea kuwaza? Je, ukiwaza huwa unawaza nini? Kiufupi; Huwa
unajisemesha nini ukiwa mwenyewe?
Utafiti wa kisayansi unaonesha kwa siku mtu
hujisemesha mwenyewe maneno kati ya 30000 hadi 50000 peke yake, kwa lugha
nyepesi tunaita Self Talk au Self Conversation au Inner Conversation. (Sauti
binafsi ya ndani, au ujumbe binafsi wa ndani unaojisemesha wewe peke yako).
Hii ni wazi kuwa haijalishi upo kwenye mazingira
gani, lakini wastani wa mawazo ya mtu au yako na yangu ni kati ya 30000 hadi
50000 kwa siku, ndivyo utafiti wa kisayansi unavyotuambia si mimi. Hatupo sana
kuchunguza wala kuongelea masuala hayo ya utafiti ila nimejaribu kutumia mfano
huo ili uwe kama sehemu ya msingi wa somo langu. Swali la kujiuliza kama mtu
anaweza kuwaza au kujisemesha maneno 50000 kwa siku, ni nini anachojisemesha?
Jiulize kama ni kweli utawaza au kujisemesha
mwenyewe maneno 50000 kwa siku hata kama hukuwahi kufanyia utafiti wa kina wa
kujua ni idadi gani, lakini swali la kujiuliza, huwa unajisemesha nini? Ni
muhimu sana kujua unachojisemesha nini kila mara hasa pale unapopata muda wa
kuwa peke yako. Maneno ya ndani unaojisemesha kila siku ukiwa mwenyewe yana
nguvu sana ya kusababisha upige hatua au kukwama kwenye maisha yako.
“Talk to yourself like
would to someone you love.”
-Brene Brown aliwahi kusema hivyo,
Bado nakufikirisha kwa swali hili; Huwa unawaza au
unajisemesha nini ukiwa mwenyewe? Huwa unaongea nini ukiwa umekaa mwenyewe pale
nyumbani, iwe ofisini, bafuni, huani, njiani, safarini, nk? Kuna watu wengi sana
wamekwama mahali si kwa sababu hawajui njia nzuri ya mahali pa kuendea bali
wamekwama kwa sababu ya kuruhusu mawazo fulani kupita ndani yao na kuyaacha
yatawale mioyo yao hata kusababisha kukwama njiani.
Siku utakayojua hakika huwa unawaza nini, na kufatilia
hatua kwa hatua unachowaza kabla ya kuendelea kuwaza, basi ndio siku
utakayofanikiwa sana maishani mwako. Na hapo ndipo utakapokuwa umeweza
kujitawala binafsi (kufanya self control) juu ya maisha yako na mazingira
yaliyokuzunguka au mazingira yoyote magumu yatakayojitokeza mbele yako. Huwezi
kushinda au kutawala hali ya nje kabla hujafahamu mipaka ya kuwaza kwako.
Mawazo ndiyo yanayoamua ukubwa wa mipaka utakayomiliki na kutawala.
Hadi pale utakapokuwa na uhuru wa kuwaza na
kutawala mawazo yako, hisia na maneno unayojisemesha kila siku ndipo
utakapokuwa na nafasi kubwa ya kuona mbele yako ilivyo (Your Self Talk
determine Your Future). Mawazo yako ya leo ndio yanayoamua utakuwa na
maisha gani baada ya miaka mitano, kumi au ishirini ijayo. Huwezi kupiga hatua
nje ya kile unachojisemesha ndani yako mwenyewe kila siku. Unajisemeshaga nini?
Je, umefatilia kila unalojisemesha linaendana na
maono uliyobeba? Je, kile unachojisemesha leo kinagusa moyo wa Mungu kwa uzuri?
Je, kile unachojisemesha huwa kinashabiana na mawazo ya Mungu juu yako? Mungu
hawezi kukuwazia mema kisha wewe ukaendelea kuyasema mabaya ndani mwako. Kila
hatua zako ni lazima ziendane na kile unachojisemea, jitabiria ndani mwako
kabla sisi wa nje kukiona. Jisemee mema.
Acha kujisemea mabaya ndani yako. Acha kukaa peke
yako na kujiwazia kushindwa wakati wote. Acha kujidharau. Acha kukaa kiupweke
muda wote. Acha kujiona mnyonge wa kila wakati na kuona kama mtu unaonewa tu.
Your a doctor of your own feelings, mind, thoughts and emotions. (Wewe ni daktari
wa hisia zako, akili na mawazo yako). Usikubali kuishi kwa kuteseka kwa mawazo
yako mwenyewe, unayo nafasi ya kubadilisha unachokiwaza muda mwingi unaokuwa
peke yako. Amua kubadilika leo.
Leo anza kupima mawazo yako na kile unachojisemesha
mara kwa mara ndani mwako, kama ni sahihi au kama kweli kinamchango wowote juu
ya ndoto na maono makubwa uliyonayo ndani yako.