Powered By Blogger

Wednesday, 25 February 2015

NDOA NA MALEZI


SOMO NDOA NA MALEZI


SEHEMU YA KWANZA





 


UTANGULIZI:


Mungu alimuumba mwanaume na mwanamke kwa mfano wake. (MWA. 1:26,27).


Wote hawa wawili walikuwa watu wa thamani sana mbele za Mwenyezi Mungu. Mungu hana mwili, kwa hiyo, ni wazi kuwa, kuwaumba kwa mfano wake (Mungu) hakumaanishi katika mwili unaoonekana wa binadamu yaani kwa nyama na damu. Bali ni ule uwezo wa kufikiri, kuchagua na kupanga. Ni katika roho, ambayo humwabudu Mungu ndani yetu na kuishi milele, ndiyo iliumbwa kwa mfano wa Mungu.


Mambo ya msingi ya ya kufahamu kabla ya kuingia au kuianzisha Ndoa,


Mungu ndiye mwanzilishi wa ndoa


Sababu mbili zilizomfanya aanzishe ndoa ni vile:-


- Alivyoona haikuwa vema huyu mtu awe peke yake.


- Mtu huyu aliyemuumba alihitaji msaidizi wa kufanana naye. (MWA. 2:18-25)


Hivyo tunaona mwanamke pia aliumbwa kwa mfano wa Mungu na ni mtu wa thamani mbele zake. Ni wazi kuwa kazi ya mwanaume na mwanamke ikawa tofauti, lakini kila mmoja anao wajibu katika kazi na huduma yake.


- Mume alipewa kazi ya kuwa kichwa yaani kiongozi katika jamaa na


- Mke alipewa kazi ya kuwa msaidizi aliyefanana naye.


Mungu akaona kila alichofanya, na tazama ni chema sana…(MWA. 1:31) …akawabarikia … (MWA. 1:28) Mungu na watu alikuwa na uhusiano kamili. Mungu alipanga kuwa ndoa na iwe ya baraka.


Kabla ya kumuumba mwanamke.


Mungu alisema na Adamu (MWA. 2:15-17). Kazi ya Adamu alipewa kuilima na kutunza bustani. Alipewa amri ya kuwa asile matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya na kuwa kama angevunja agizo kifo kingemkabiri.


 


Dhambi ya Adamu na Hawa.


Walikula matunda walioambiwa wasile (MWA. 3:1-6) Matokeo yake: - Mungu alimlaani nyoka kwa udanganyifu (MWA. 3:14). Akatoa adhabu kwa Hawa na kisha adhabu kwa Adamu. (MWA. 3:16-19).


Kwa sababu ya dhambi uhusiano kamili uliharibika.


Adamu na Hawa wakajikuta hawana uhusiano mzuri na Mungu, wakajificha. Lakini Mungu alikuwa na mpango endelevu, ambayo ilikuwa habari njema kwa hawa watu wawili. (MWA. 3:15). Akatoa Ahadi ya kwamba uzao wa mwanamke utamponda kichwa huyo nyoka. Hiyo ni ahadi ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo ambaye alimshinda shetani kwa njia ya msalaba. Mungu alitumia mwanamke kama daraja katika kumleta Yesu ambaye amefanyika upatanisho katika kumuunganisha mtu na Mungu. Hivyo Yesu aliimarisha thamani ya mwanamke na kumpa heshima sawa na mwanaume.


2. NDOA YA KIKRISTO


Inaitwa ndoa ya Kikristo pale mume na mke wameoana na kujenga unyumba wao katika misingi ya Kibiblia / Kikristo. (2KOR. 6:14-15) Wakristo ambao wanatunza ushirika mzuri na Mungu. (1YOH. 1:5-7, MT. 6:33).


Mpango wa Mungu kwa wana ndoa ni kuona kila mmoja anachukua hatua ya:


i). Kuacha baba na mama yake


ii). Kuambatana na mwenzi wake


iii). Kuwa mwili mmoja.


Huu ni ushirika na msingi mzuri na wa muhimu kwa mume na mke Mkristo. Pia Mungu aliwataka mume na mke kuzaa watoto kupitia ndoa yao. Ijapokuwa kuzaa watoto sio sababu ya kwanza kwa msingi wa ndoa, hayo ni matokeo tu ya baraka katika ndoa.


Sababu kubwa ni mume na mke wapate mapenzi ya ushirika wao pamoja katika maisha yao, wakionyesha kupendana, kukaa kwa umoja, kushirikiana na kutunza mahusiano mazuri na Mungu na wao wenyewe katika kutimiza mapenzi ya Bwana. Ndoa isiwe sehemu ya majuto, bali, furaha amani na baraka.


 


3. NDOA, KRISTO NA KANISA.


Uthamani wa Ndoa, Bwana Mungu amelinganisha kwa mfano wa vile anavyoliona Kanisa na Kristo. Amelinganisha na Bwana arusi na Bibi arusi, ya kuwa Kanisa ni Bibi arusi wa Kristo, na Yesu Kristo kuwa ni Bwana arusi. (EFE. 5:22-23, UFU. 21:2, 22:17). Kila mmoja kwa upande wake anaowajibu wa kuona mpango huu wa Mungu unafanikiwa ulivyokusudiwa, kama vile Kristo Bwana arusi anaendelea kuhusika na Kanisa (YOH. 14:1) na pia Kanisa kama Bibi arusi linatakiwa kufanya yanayolihusu. (UFU 19:7,8)


i). Amri za Mungu kwa Wanaume. (EFE. 5:25-33)


a]. Mume anapaswa kumpenda mke wake.


Imelinganishwa na vile Kristo anavyolipenda kanisa, tena kama mtu anavyoupenda mwili wake mwenyewe. (EFE. 5:25,28,33, KOL. 3:19) Neno lasema, “Imewapasa wanaume kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe, ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe”. Kuwa na upendo kama ule wa Kristo, mume atasema, nampenda mwanamke huyu kiasi cha kutosha nijitoe kuwa sadaka kwa ajili yake. Nataka nimtunze na kumlinda. Nataka kushirikiana naye maisha yangu yote. Hakuna atakayekufanyia mkeo aweze kuendelea kuwa mzuri, isipokuwa wewe peke yako.


Kabla hujamuoa, wazazi walihusika kumtunza na kumjali, akapendeza kimaadili na maumbile, ukampenda. Sasa basi, ni wajibu wako hasa kuona yale uliyoyapenda yanaendelea, wala mume usifike mahali pa kuona sasa hakufai kwa sababu ati hayuko kama vile mwanzo mlivyooana. Ni mke wa ujana wako mpende. (MAL. 2:14-16) “... Kwa hiyo jihadhari roho zenu, mtu awaye yote asimtende hiana mke wa ujana wake. Maana mimi nakuchukia kuachana asema Bwana ...” (1KOR. 13:4-8)


b]. Mume ni kichwa cha mkewe.


Kama vile Kristo ni kichwa cha kanisa yaani kiongozi mkuu wa kanisa ndivyo mume pia Mungu anamtaka awe kiongozi wa mkewe katika jamii. Anawatunza, anafanya maamuzi ya hekima na kuwa mfano mwema kama kiongozi. Anamjali mkewe na kumshirikisha kama msaidizi wake katika uongozi kwa maisha yake yote na wala si mtumwa au mfanyakazi wake (MK. 10:42-45).


c]. Kristo ni kichwa cha mume. Mume yupo chini ya Kristo (1KOR. 11:3)


Kristo anamtaka kila mume kuonyesha upendo kwa mkewe:


- Kumpenda (KOL. 3:19),


- Kumheshimu (1PET. 3:7).


Mwili wa mwanamke ni dhaifu kuliko wa mwanaume, Mungu alimfanya mwanamume kuwa na nguvu zaidi ili aweze kutunza jamii yake – asiwe mkali (KOL. 3:19, KOLl. 3:13), kuwa mkali, kuna maana ya kunena maneno ya hasira na kumlaumu mtu. Katika maisha ya kila siku, lazima mume awe mvumilivu kwa mkewe, anapaswa kumsamehe anapokosea na amsaidie afanye mema inavyoshahili. Mume aambatane na mkewe. (MWA. 2:24, MK. 10:7, MT. 19:5).


Kabla ya ndoa, maisha ya mwanamume yanafungiwa pamoja na wazazi wake. Baada ya kuoa, anapaswa maisha yake yafungamane au kuambatana pamoja na mke wake:


- kufungwa pamoja au kushonwa pamoja naye


- kushikamana kama kitu kilichogundishwa na gundi


- mume na mke wanakuwa kitu kimoja (MT. 19:6)


- kuonyesha ushirika katika sehemu zote za maisha.


ii). Amri za Mungu kwa Wanawake. (EFE 5:22-24,33)


a]. Mke anapaswa kumheshimu (kumstahi) mumewe.


 


- Hii ni kwa sababu mume ni kichwa chake au kiongozi wake.


- Pia kwa sababu yapo mema ndani yake (mume) kwa ajili yake (mke).


Heshima yake inampa mumewe nguvu nyingi za kuongoza na kufanya kazi yake, pia heshima yake inamfanya mumewe kutukuka na kuwa mjasiri kwa jamii yake. (MIT. 31:10-12,23-29) “Mke mwema nani awezaye kumwona?... Moyo wa mumewe humwamini, wala hatakosa kupata mapato. Humtendea mema wala si mabaya, siku zote za maisha yake… Mume wake hujulikana malangoni, aketipo pamoja na wazee wa nchi… Hufumbua kinywa chake kwa hekima ... Wanawe huondoka na kumwita heri, mumewe naye humsifu..”


Kinyume cha kutomheshimu, mumewe hudhoofika kifikra na kujiona duni kwa familia yake na jamii na hivyo kuathiri maisha mazima ya kindoa na hatimaye ndoa kuwa hatarini siku kwa siku.


b]. Mke anapaswa kumtii mumewe. (EFE. 5:22)


- Maana ya – stahi - ni wekea heshima, wekea adabu, heshimu


- na - tii - ni fanya ilivyoamriwa, au fuata amri.


Hivyo mke anapaswa kujifunza kutii na kufanya hivyo kwa hiari kwa sababu anajua ni wajibu wake na si kwa kulazimiswa. Utii unaotoka ndani uliambatana na upendo unaleta harufu nzuri ya manukato kwa mumewe. Hii si kwa sababu mke si muhimu kuliko mume, bali ni mtililiko wa maisha yao katika mfumo wa amani Mungu aliufanya.


Askari ni lazima ajifunze kutii ili kukidhi ufanisi bora wa kazi yake na bila kufanya hivyo si rahisi kufanikisha majukumu ya kiaskari. Hivyo ndoa isio na utii wa mke sio rahisi kuleta ufanisi wa maisha ya furaha katika ndoa yao.


Hapaswi kufanya kama mtumwa. Lakini Mungu anamwamuru mke utii kwa sababu ni mpango bora aliouweka ili kukidhi kanuni kimaongozi, kwa wanandoa ili kuipa furaha, amani na mafanikio mema. Pasipo Utii kwa kiongozi hakuna mafanikio ya uongozi mahali popote duniani na mbinguni. Mwenendo wa mke mwema, mtii unamvuta mumewe kwa Kristo. (1PET. 3:1,2)


c]. Mke anapaswa kumpenda mumewe (TIT. 2:4)


 


Neno la Mungu linaagiza wake kuwapenda waume zao. Wanapaswa kuwa na upendo wa Kristo ndani yao. Upendo kati ya mke na mume huwapa watoto nguvu na maisha ya furaha nyumbani. Panapo upendo pia kusameheana kunakuwepo. Mkasameheane kama Kristo alivyowasamehe. (Kol. 3:12) Kwa kila kosa pasipo kuhesabu au kulimbikiza mabaya moyoni. Hata kama ukiwa na sababu, samehe, huo ni upendo halisi wa kimungu ‘agape”. (1KOR. 13:4-8)


d]. Mke anafanya maisha ya jamii nyumbani kuwa mema. (TIT 2:3-5)


Jamii ya Kikristo inapaswa kuwa na maisha mema, yenye upendo, amani, ushirika na mafundisho yenye maadili ya Ukristo. Jamii inajisikia kufarijika kuwepo nyumbani kwao. Watu wengine wanapoona maisha mema ya Kikristo, wanavutwa kwa Bwana na kumtukuza Mungu.


- Kazi ya kufanya mazingira na maadili bora ya Kikristo nyumbani, huleta heshima kwa jamii husika.


 


- Watoto wanajifunza nyumbani njia za Mungu toka kwa wazazi wao.


- Mke kama kiungo muhimu cha jamii nyumbani, anafanya jamii / watoto kushiriki mema ya mumewe na kwamba wajisikie salama, amani na furaha.


iii). Jitahidi kuhifadhi Umoja (EFE. 4:2,3)


Mume na mke lazima wajitahidi kuuhifadhi umoja wao katika kifungo cha amani, ili maadui wa nje na ndani wa ndoa yao wasije wakapata nafasi, na kuweza kumshawishi vibaya mmoja wao na kuleta shida katika ndoa yao.


Eva alipokuwa akitembea peke yake katika bustani alipata nafasi ya kuongea na nyoka, adui wa ndoa na nyoka kufanikiwa kumshawishi Eva vibaya. (MWA. 3:1-6) Hivyo, umoja wa kwanza wa wanandoa unaweza kuvunjika kwa kuacha mianya hiyo. Adamu anaanza kumlaumu Hawa, ni huyu mwanamke! (MWA. 3:12) Wanandoa wanaweza wakaendelea kuishi pamoja, lakini ukuta ukawa kati yao. Tunapaswa kufikiri! Jambo gani linaweza kuharibu umoja wetu wanandoa, mume na mke?


* Njia ya kuhifadhi umoja (FIL. 2:1-4)


Wanaweza kujihoji tufanye nini ili tuhifadhi umoja wetu?


- Neneni wazi ninyi kwa ninyi, ni lazima waelezane mawazo yao wao kwa wao. Wanaponena wazi watakuwa wakichukua hatua ya kufikia umoja. Pia wanaponena wazi kila siku, inaondoa mashaka na kutoaminiana kati yao. (1YOH. 1:7)


- Iweni radhi kukubali mawazo ya kila mmoja wenu, bila kuona mwingine ni bora kuliko mwenzake, hivyo kudharau wazo lake. Mume na mke lazima wawe na shukurani wao kwa wao na kuheshimu mawazo ya mwenziwe.


- Jitahidini kupata jibu linalokubalika na kujenga. Kupata jibu zuri kuna maana kumbwa, lazima wote wawili wajaribu kukubaliana.


- Kutiana moyo (EBR. 10:24). Wakati mwingine mume au mke anapata shida za maisha kuwa nzito sana kwake, anajisikia kukata tamaa, kuchoka katika jambo fulani. Inaweza kuwa mambo ya kazini, jamaa au majirani kuja kinyume, huduma nk yapasa kutiana moyo na kuombeana. Unaweza kumtia moyo kwa neno la upole, unyenyekevu, maneno yenye kukolea munyu na baraka (KOL. 4:6, EFE. 4:29) na kufariji ili mwenzi wako apate kuendelea vizuri. Hayo yanajenga umoja zaidi.


- Mke lazima ajaribu kukubali mpango wa mumewe


- Mume lazima ahakikishe mkewe anamuelewa katika hilo na ni kwa faida ya familia yake


- Pia kwa kutumia maombi kuwa njia kufikia muafaka kwa mambo magumu baina ya wanandoa. 


Mungu ni jawabu la mambo mengi pale unapomshirikisha, maana yeye ni kiini cha ndoa ya Kikristo (ZAB. 37:5-7, ISA. 26:3,4,9)


* Sema kweli katika upendo na mwenzi wako. (EFE. 4:25,15)


“Basi uvueni uongo mkaseme kweli kila mtu na jirani yake... tuishike kweli katika upendo na kukua..” Jirani wa kwanza ni mume au mke wako. Ili ndoa idumu na kukua, na pia kuendelea vizuri, sema kweli katika upendo na mwenzi wako. 


Kusema kweli katika upendo, kunasaidia kuondoa jaziba, ghadhabu, hasira na hatimaye mabishano na magomvi ya nayo zaliwa na hayo. ”Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja nakila namna ya ubaya” (EFE. 4:31) Jiepushe na mabishano, ubishi katika ndoa huleta uchungu na kujenga chuki baina yenu pia na jamii yako.


* Kunena mamoja.


Jamii ya Kikristo inapaswa kuwa mfano mwema wa kuishi kwa ulimwengu. Yapaswa kuonyesha jinsi Kristo apendavyo kanisa na jinsi kanisa limpendavyo Kristo. Yapaswa kuonyesha jinsi Mungu atakavyo Wakristo waishi.


- Wanaweza kushirikiana mambo yaliyotokea.


Usiku na wakati wa mapumziko mazuri, muda wa utulivu ni muhimu sana kuelezana mambo ambayo yametokea wakati wa mchana. Wakati huu wanapata nafasi ya kujifunza toka kwa kila mmoja kwa kushirikia habari ambazo wamesikia. Unapotumia muda ambao mwenzi wako amechoka au katingwa na shughuli nyingi katika kuwakilisha mambo muhimu, unafanya yasitiliwe maanani na kulaumiana katika utekelezaji. Njia hii haifai kabisa.


- Wanaweza kusema shukurani zao.


(2THE. 1:3,4 FIL. 1:4,5, 4:14) Hii inamaana kwamba tunaweza kuwaambia waume au wake zetu mema tunayoyapenda kuhusu yeye. Kumpongeza mwenzi wako ni muhimu na kumwambia nakupenda, anatamani kusikia toka kwako neno la faraja na shukurani.


- Wanaweza kuonyana. 


(EBR. 3:13 GAL. 6:1) Ni muhimu wanandoa kusaidiana katika kila jambo, na kumlinda mwenzi wake na mabaya. Hivyo ni vizuri kabisa kuonyana kwa upendo pale mume au mke anapoenda katika mwelekeo usiofaa, kuliko kungoja mambo yaharibike na kuishia kulaumiana na kuishia vibaya na majuto kwa ndoa na jamii yenu.


4. KUISHI VEMA PAMOJA


i). Kufanya mambo pamoja.


Machoni pa Mungu, jamii ya Kikristo ni kitu cha ajabu sana. Mume na mkewe ni picha ya Kristo na kanisa. Mume anapaswa kuwa kama Kristo na mke anapaswa kuwa kama kanisa. 


Katika Warume 8:29 imeandikwa: “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao... katika kuwapatia mema …” Mume na mke wanapofanya kwa pamoja na ushirikiano mzuri, ni rahisi kulitimiza kusudi lao la maisha. Huwasaidia kuondokana au kujilinda na migongano na malaumiano yasio ya lazima. Kila mmoja wao ana kazi yake ambayo inamfanya ashughulikie wakati mwingine. Hata hivyo ni muhimu kwamba wafanye mambo mengine pamoja.- Shughuli za kiroho.


Kuna njia nyingi ambazo mume na mke wanaweza kuwa na ushirika katika shughuli za kiroho mfano katika:


- Kusoma Biblia.


- Kuombeana.


- Kwenda kanisani pamoja.


- Kupata mafunzo ya Biblia pamoja.


- Kumtumikia Mungu pamoja kwa mfano wa Prisila na Akila. (MDO. 18:1-3,26, Rum. 16:3)


- Shughuli za nyumbani.


Hii ni pamoja na kufanya kazi pamoja shambani, kufanya kazi pamoja katika kutengeneza na kusafisha nyumba, kwenda kununua mahitaji ya jamii. Pia wawashirikishe watoto katika shughuli za nyumbani.


ii). Tunapokosewa. (MT. 5:23,24, EFE. 4:31,32, KOL. 3:13, MT. 18:15, GAL. 6:1)


Moja wapo la matatizo yanayozuia mume na mkewe wasiwe na umoja ni tatizo la kukosewa. Kama umekosewa na mwenzi wako, tafuta kupatana upesi, msamehe, nena pamoja kwa roho ya upole. Mungu anatutaka tupatane na kusameheana katika makosa yetu kabla hatujamwendea kumwabudu.


Anasema, ”Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu, iache sadaka yako, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako kisha urudi utoe sadaka yako”. “Mchukuliane na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake kama Bwana alivyowasamehe ninyi vivyo na ninyi”.


Tabia ya kiburi ndicho kinafanya kuzuia kupatana na kuomba msamaha kwa makosa yetu upesi. (MIT. 11:2) “Kijapo kiburi ndipo ijapo aibu, bali hekima hukaa na wanyenyekevu”. Ni lazima Tunda la Roho katika maisha yetu lionekane na ni muhimu sana. (GAL. 5:22,23)


iii). Ndoa na asiyeamini. (1PET. 3:1,2)


Ndoa za namna hiyo zinaweza kuwa na matatizo mengi. Mkristo anaweza akaoana na mtu asiyeamini kwa sababu mbalimbali:


- pengine yeye alimpokea Kristo baada ya kuoana.


- pengine yule asiyeamini alijifanya kuwa ni Mkristo kabla ya ndoa.


- pengine Mkristo alioana na asiyeamini kwa kupenda kwake.


Unaweza kuwaambia nini vijana ili kuwasaidia wapate kweli kuhusu yule atakaye kumwoa? Ni muhimu wakashauriwa, ili waombe Mungu kwanza. (EZR. 8:21) “Ndipo nikaamuru kufunga ... ili tupate kujinyenyekeza mbele za Bwana, na kutafuta kwake njia iliyonyooka ...” (MIT. 19:14) “Mke / mume mwenye busara au mwema mtu hupewa na Bwana”, Watafute ushauri kutoka kwa wale


wanaomjua msichana au mvulana husika. Wachukue muda kunena pamoja kuhusu mambo ya kiroho. Pia wasome Biblia na kuomba.


Katika waraka wa Petro, anasema, asiyeamini anaweza kuvutwa na mwenendo wa mkewe. Matendo mema ya mkewe ni masomo kwa mumewe. Anapoona matendo yake mema anafikia uamuzi wa kumtaka Kristo awe Mwokozi wake. Mke anapaswa kumheshimu mumewe kwa sababu yeye ni kichwa au kiongozi wake. Lakini mke / mume atafanya nini mwenzi wake anapomtaka kufanya jambo lililo kinyume cha Biblia? Mkristo lazima atii amri za Mungu ili aishi maisha ya kumpendeza Mungu na mwenzi wake. (1PET. 5:29)


iv). Kuwa na jamaa wengine.


Wanandoa ni wazi kuwa wanaingia katika maisha na jamii nyingine ambayo inaweza ikawa si Wakristo toka kwa mume na mke. Jinsi gani mume na mke wakawa nuru njema kwa jamii hiyo:-


- Kwa kuonyesha upendo na matunzo mema kwa jamii yao. (1TIM. 5:8) “Lakini mtu yeyote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini”.


- Kuwa na moyo wa kumpendeza Mungu katika maisha yao.


- Kutoa msaada kwa jamii.


- Kujitenga mbali na dhambi na uovu katika jamii hasa tamaa mbaya na uasherati. (2KOR. 6:17,18)


- Hawapaswi kuonyesha ubaguzi katika jamii wanayoishi nayo aidha kwa sababu ya jamii hiyo ni ndugu wa mume au mke.


JE? UKO TAYARI KURUDISHA NDOA YAKO KATIKA MAHUSIAMO NA MUNGU  NAJUWA UKO TAYARI FANYA MAOMBI SASA


 


SOMO NDOA NA MALEZI


SEHEMU YA PILI
 


Utangulizi:


Ninapoongelea maisha ya ndoa ninamaanisha kwamba Ndoa inahitaji kutuzwa isije ikafa au ikaishia njiani,


 HAKI YA WANA NDOA.


“Kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe. Mume na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake. Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe; vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake, bali mkewe. Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali, (kumudu maisha ya wokovu), mkajiane tena, shetani asije akwajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu.” (1KOR. 7:2-4).


Ni wazi kuwa mume na mke kama wanandoa, wakaipoteza haki yao; heshima hii waliopewa na Mungu, juu ya tendo la ndoa, basi, tatizo kubwa litakuwa limewaingilia. Pamoja na kupeana, vitu vizuri, kusaidiana, kuhudumiana, kupendana, kuishi katika nyumba moja nk. 


Bado, pasipo kushirikiana katika tendo la ndoa ni hatari, huwafanya hawa mume na mke kuwa kama ndugu wengine wowote tu wanaoishi nao, yaani, dada, kaka, watoto, na jamaa nyingine iliyopo. Madhara yake tunaona huwa makubwa na haya ufa huanza taratibu. Upendo wa kwanza na mahusiano baina yao hupungua siku kwa siku. 


Hatimaye hamu ya kutafuta mpenzi mwingine atakayekidhi haja hiyo huingia, na hivyo, kusababisha mume au mke kutenda tendo hilo nje ya ndoa yake.  Ili lisitoke tatizo hilo hakikisha kabla ya kufanya tendo Hilo maombi kwanza,ndipo uanze kufanya mapenzi.


Ni kweli, huduma zingine anaweza kuzipata nje ya ndoa yake, kama vile, chakula – ataweza kula hotelini, nguo - zikafuliwa na dobi, usafi - ukafanywa na msichana wa kazi nk. Lakini tendo la ndoa ni haki pekee ya wanandoa, yaani, mume na mke wake. Na kufanya kinyume cha hayo ni kuasi agizo la Mungu.


Kwa nini mume au mke anaweza kwenda nje ya ndoa?


Sababu zinawe kuwa kama maandiko yanavyoeleza ya kuwa:-


- Kunyimana


- Kuwa na amri juu ya mwili wake (matakwa yake binafsi, bila ya kujali mwenzake)


- Tamaa mbaya


Hayo ni mambo ambayo Biblia imeyaainisha. Na hayo huweza kusababishwa na mmoja wao katika ndoa aidha mume au mke. Wanawake wengi hupenda kutumia kutoa adhabu kwa waume zao kwa kumnyima tendo la ndoa (moyoni anasema tutaonana kitandani! Utakoma ubishi!), hasa inatokea mara anapojisikia kukwazika na kuona hawezi kumsamehe kabisa, basi, anaona njia pekee ni kufanya hivyo. Kwa ujinga huo kusababisha mwenzi wake kujaribiwa na wapenzi wengine wanaoonekana kuwa kumpenda na kumhudumia vizuri. 


 


Biblia inasema, “Mungu ameumba jambo jipya duniani, mke atamlinda mwanamume.” (YER. 31:22). Ataweza kumlinda hasa mumewe? Jambo kuu ni yeye kuona anampa haki yake inavyostahili. Vivyo wanaume wengi kwa kutokuonekana muda mwingi mbele za wake zao kwa visingizio vya shughuli nyingi nk, hutoa nafasi kwa wanawake kushawishika na waume wengine ili kushiriki tendo hilo. Wazo lao, huenda linawajia kuwa nitafanya mara moja tu kwa leo, na maadamu mume au mke wangu asijue. 


Lakini kwa kujaribu kufanya hivyo, mara, anajikuta anajikuta ameanguka na kuvunja uhusiano wake na Mungu, uovu umeingia na kummiliki. Na hatimaye wanandoa wenyewe hujikuta kudhoofika kiimani, na mahusiano yao binasi. Pia ni hatari kubwa kwa maambukizi ya VVU na IKIMWI kwa jamaa, na kuleta shida kubwa kwa familia na watu wengine. 


Kwa hiyo wanandoa wanashauriwa kuhakikisha kuwa hawanyimani tendo la ndoa kwa visingizio viwavyo vyote, kama, makwazo, chuki, kukosa vitu, kinyongo na mengineyo yasiyo ya lazima, kama vile, mwanamke kuwa katika siku zake (Law.15:19,25), magonjwa nk. 





**************************************************************

Ninawezaje Pata amani?

Unawezaje kupata amani? Baba Nabii akifunua siri ya kuwa na amani kama ya kwake aliyonayo Utangulizi kazi kubwa kabisa kwa Mwanadamu...